Ofisi ya Chadema iliyochukuliwa na CCM hii hapa
Makada na viongozi wa Chadema kata ya Ruaha wakitazama bango la safu ya uongozi wa Chadema
katibu wa CCM kata ya Ruaha Rashid Shungu ( wa pili kushoto ) na kada wa Chadema aliyehamia CCM Ibrahim Mmasi pamoja na wanachama wengine wa CCM wakiwa wameshika bendera ya CCM ambayo itapepea katika ofisi mpya ya kata ya Ruaha ,ofisi ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na Chadema kabla ya kufukuzwa kwa kushindwa kulipa deni la kodi kiasi cha Tsh 540,000 , kushoto fundi rangi akiendelea kupaka rangi ya CCM.(Martha Magessa)
CHAMA cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kata ya Ruaha jimbo la Iringa mjini kimepata pigo kubwa baada ya kufukuzwa katika nyumba waliyopanga kama ofisi ya kata hiyo baada ya kushindwa kulipa deni la pango kiasi cha Tsh 540,000 walizokuwa wakidaiwa na mwenye nyumba deni ambalo limelipwa na Chama cha mapinduzi (CCM ) kata ya Ruaha kabla ya kuichukua ofisi hiyo .
Mmiliki wa nyumba hiyo iliyopo mtaa wa Ngeleli Ipogolo Bi Neema Mwasika alifikia hatua hiyo ya kuwataka kuondoka katika ofisi hiyo baada ya jitihada za kudai deni lake kushindikana na hivyo kulazimika kupangisha nyumba hiyo yenye chumba kimoja na sebure kwa mpangaji mpya ambae ni CCM kata ya Ruaha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katibu wa CCM kata ya Ruaha Rashid Shungu alisema kuwa awali CCM kilikuwa na ofisi yake eneo la Ruaha jirani na mto hivyo kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana zilipelekea ofisi hiyo kuharibiwa vibaya na hivyo kukosa kabisa ofisi .
Alisema kuwa kutokana na kutokuwa na ofisi cham a kilikuwa kikitumia nyumba ya mtu binafsi kama ofisi pale ilipohitajika kukutana viongozi ama wanachama .
Shungu alisema kuwa jitihada za kutafuta nyumba ya kupanga ili kutumika kama ofisi ya muda ya CCM kata hiyo ya Ruaha ziliendelea kufanyika chini ya aliyekuwa kada wa Chadema kata hiyo kabla ya kujiunga na CCM Bw Ibrahim Mmasi
Hata hivyo alisema ofisi hiyo alisema kuwa baada ya kuona ofisi hiyo imefungwa kwa muda na kuwasiliana na mwenye nyumba alikubali kuwapangisha kwa makubaliano ya kulipa deni kwanza jambo ambalo lilifanyika hivyo na kulipia kodi ya miaka miwili zaidi.
" Tumeipata ofisi hii kihalali na sio hujuma kwani makubaliano kati ya mmiliki wa nyumba na mpangaji yalifanyika na hivyo kwa kuwa hitaji letu nyumba ya kupanga tuliona hiyo ina sifa ambayo tuliitaka hivyo tunachofanya ni kufuta rangi na nembo za Chadema na kuweka rangi ya CCM na nembo zetu .....na tutaizindua rasmi jumapili wiki hii"
Kwa upande wake kada wa CCM aliyehama kutoka Chadema Bw Mmasi alisema kuwa ofisi hiyo ilikuwa imezinduliwa na viongozi wa kitaifa kupitia zoezi la oparesheni Sangara tarehe 19 mey 2011 chini ya naibu mkuu wa Chadema enzi hizo Zitto Kabwe na mbunge wa jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa na viongozi wengine .
No comments:
Post a Comment