Wednesday, September 30, 2015

MAGUFULI: MAFISADI HAWATAKI NIINGIE IKULU… ASEMA HAWAWEZI KUMPIGIA KURA KWA KUWA WANAMUOGOPA



MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli, amesema mafisadi hawawezi kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa wanamwogopa.
Dkt. Magufuli aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara,uliofanyika katika Viwanja vya Mvumi Misheni, Jimbo la Mtera,mkoani Dodoma.
"Mafisadi hawawezi kunichagua kwa sababu wananiogopa ila wapo Watanzania wengi wanaonipenda na kunikubali wakiwemo maskini wenzangu, wanyonge ambao watanipa kura nyingi ili niweze kuwatumikia na kutetea masilahi yao," alisema.
Alimpongeza mwanasiasa mkongwe, Mzee John Malecela kwa ujasiri wake wa kuendelea kubaki CCM licha ya kushindwa katika mbio za kuwania nafasi ya urais miaka iliyopita.
"Mzee Malecela aliwahi kugombea uteuzi wa nafasi ya urais, lakini hakufanikiwa na hakufikiria wala kuthubutu kuhama chama hata siku moja, bado yupo na amekuwa msaada mkubwa," alisema.
Alisema mbali ya kuukosa urais, pia aliangushwa kwenye nafasi ya ubunge wa Jimbo la Mtera na Livingstone Lusinde lakini hakuhama chama. Alisema anawashangaa waliohama CCM baada ya kukosa nafasi.
Aliwaomba Watanzania wamchague aweze kubadilisha maisha yao na kukuza uchumi akiwataka wasikubali kudanganywa na wapinzani ambao hawana sera wala uzoefu wa kuongoza Serikali.
Akizungumzia sera ya elimu bure, alisema hakuna sababu ya kukosa madawati wakati nchi ina rasilimali kubwa ya miti; hivyo alitoa wito kwa Wakurugenzi kukaa mkao wa kufanya kazi.
Livingstone Lusinde 
Naye Mjumbe wa Kamati ya Kampeni za CCM na mgombea ubunge Jimbo la Mtera, Lusinde alisema CHADEMA kimepoteza mwelekeo baada ya kuwapokea wanasiasa waliowatuhumu kwa kashfa mbalimbali ndani na nje ya Bunge.

No comments:

Post a Comment