Wednesday, September 30, 2015

Sifa Kubwa 10 Kudhihirisha kuwa CCM ni Chama Bora Barani Afrika




1. CCM ni Chama chenye mtandao mpana mpaka ngazi zote za chini nchi nzima. Kiongozi wa chini kabisa katika jamii yetu ni mjumbe wa shina wa CCM. Kabla ya kumwona kiongozi yeyote katika ngazi ya chini, wa kwanza kumwona ni kiongozi wa CCM. Hakika ni mtandao pekee mpana barani Afrika!
2. CCM ni Chama kilichohimili na kustahimili mikikimikiki na misukosuko ya mabadiliko ya kisiasa pasipo kuyumba wala kutetereka. Vyama vingine vikongwe vimesambaratika vibaya. Mathalani UNIP cha Zambia, MCP cha Malawi, KANU na NARC vya Kenya, NDC cha Ghana, Socialist Party (PS) cha Senegal na SLPP cha Sierra Leone, na vinginevyo. Hakika huu ni uimara na umadhubuti wa pekee barani Afrika!
3. CCM ni Chama kilichoonesha uwezo na ukomavu mkubwa katika kusuluhisha migogoro na tofauti ndani ya Chama kwa njia za amani, maelewano, maridhiano na kusameheana kupitia vikao halali vya Chama. Hakika hii ni demokrasia ya pekee na ya kuigwa barani Afrika!
4. CCM ni Chama kilichoweza kubadilishana viongozi kwa mchakato ulio wazi, wenye ustaarabu mkubwa na wa demokrasia ya kweli ndani ya Chama na Serikali, pasipo uhasama wala vurugu zozote tokea Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere alipong’atuka 1985, na tokea mfumo wa vyama vingi ulipoanza upya 1992. Hakika hii ni historia pekee na ya kuigwa barani Afrika.
5. CCM ni Chama kilichomudu kuimarisha na kuviwezesha vyama vingine kukomboa nchi zao kusini mwa jangwa la Sahara. Mathalani FRELIMO cha Msumbiji na MPLA cha Angola (1975), ZANU-PF cha Zimbabwe (1980), NRM cha Uganda (1986), SWAPO cha Namibia (1991) na ANC cha Afrika Kusini (1994), na vinginevyo. Hakika huu ni mchango mkubwa na wa kipekee katika historia ya ukombozi wa Bara la Afrika.
6. CCM ni Chama chenye kutetea, kulinda na kuimarisha amani, utengamano na umoja wa kitaifa nchini, na kuleta maelewano baina ya vyama, sambamba na viongozi wake kujihusisha bega kwa bega katika kuyapatanisha makundi yanayohasimiana katika nchi jirani na kwingineko barani Afrika. Hakika huu pia ni mchango wa pekee barani Afrika!
7. CCM ni Chama chenye uzoefu mkubwa wa kuwekeza na kuendesha miradi ya maendeleo inayolenga kuinua uchumi wa wananchi na kuhakikisha uwepo wa ulinzi na usalama wa mali zao. Hii ni pamoja na kulinda na kuhifadhi magari ya thamani kubwa pasipo kujali itikadi za wamiliki. Hakika huu ni uzalendo na utaifa wa pekee na wa kuigwa barani Afrika!
8. CCM ni Chama kilichoweza kutoa viongozi mahiri na waliotukuka katika ngazi ya kitaifa na Kimataifa kwenye nyanja mbalimbali. Mathalani kwa uchache, Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere, Hayati Edward Moringe Sokoine, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro, Salim Ahmed Salim, Balozi Ali Mchumo, Rais wa Bunge la Afrika Getrude Mongella na wengineo. Hakika hii ni sifa ya pekee na ya kujivunia barani Afrika!
9. CCM ni Chama kinachohamasisha wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya kila siku pasipo kusubiri nyakati za uchaguzi. Tunawaona viongozi wa CCM wakituhimiza kila siku kufanya kazi kwa bidii. Hakika jambo hili ni nadra sana kuliona kwingineko barani Afrika!
10. CCM ni Chama kilichoonesha dhamira ya kweli kuhusisha na kuutambua mchango wa wanawake katika vyombo mbalimbali vya maamuzi, ikiwa pamoja na uwepo wa wanawake wa kutosha katika Baraza la Mawaziri na kuwapa vyeo vya juu jeshini. Hakika huu ni mfano pekee na wa kuigwa barani Afrika katika usawa wa kijinsia.

No comments:

Post a Comment