Wednesday, September 2, 2015

WAZEE SONGEA WAMUANGUKIA RAIS AJAYE

WAZEE wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wamemtaka mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye uchaguzi mkuu ujao kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais wa nchi kwa awamu ya tano wazee wa Tanzania wanamuomba aone umuhimu kwa kutambua mahitaji yao na kuwasaidia changamoto walizonazo.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa baraza huru la wazee wa halmashauri ya manispaa ya songea Salum Mwale wakati akichangia mada kuhusu mahitaji na matarajio ya wazee wa Tanzania iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali linalowahudumia wazee (PADI) lenye makao makuu mjini songea kwenye mkutano uliowakutanisha wazee na waandishi wa habari.

Mwale alisema kuwa wazee kwa muda mrefu wamelitumikia Taifa la Tanzania katika sekta mbalimbali zilizo rasmi na zisizo rasmi na wamekuwa chimbuko kubwa na mhimili wa taifa la Tanzania wamekuwa wakitoa jasho jingi katika kuhakikisha kuwa taifa linasonga mbele lakini bado wanaendelea kutoa mchango wao kwa kujinyima sana hasa ikizingatiwa hali zao za kiuchumi ni mbaya sana.

Alisema kuwa ili kuhakikisha vijana wanapata elimu na maisha bora kwa lengo la kuboresha uchumi wa nchi kwa kizazi kijacho bado wazee wanaendelea kuuumia na serikali haionyeshi kuwasaidia kwa kuwapa pensheni.

Hivyo amemuomba rais ajaye wa serikali ya awamu ya tano kazi kubwa ya kwanza atayoanza kuifaanya ni vyema aangalie namna ya kuwasaidia wazee kwa kuhakikisha kuwa wanapatiwa pensheni ambayo itapunguza kwa kiasi kikubwa baadhi ya changaamoto wanazokabiliana nazo.

Kwenye mkutano huo uliofanyika kwenye kituo cha kulelea wazee kilichopo eneo la Unangwa nje kidogo ya manispaa ya songea Edita Nchimbi ambaye ni mjumbe wa babraza huru la wazee wa manispaa ya songea alisema kuwa pensheni kwa wazee ni muhimu sana hivyo ni vyema serikali ijayo ikachukua jukumu la kuwatambua wazee wote hapa nchini kwa kuwapa huduma mbalimbali zikiwemo za matibabu kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za serikali.

Kwa upande wake Daud Mpangala ambaye pia ni mjumbe wa baraza la wazee ameiomba serikali ya wamu ya tano itakapoanza kufanya kazi isikilize kilio cha wazee wanaohitaji kusaidiwa kupatiwa pensheni na huduma zingine tofauti na ilivyo sasa wazee wamekuwa wakikabiliana na changamoto nyingi kwa vile hawana uwezo kiuchumi.

No comments:

Post a Comment