Mgombea mwenza wa urais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), anayewakilisha umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) Mh. Juma Duni Haji amesema iwapo watanzania watamchagua mgombea urais wa chama hicho, serikali itahakikisha angalau barabara zote zinazounganisha wilaya moja na nyingine katika mikoa ya Lindi na Mtwara zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima pamoja na kuchochea kasi ya uwekezaji wa ndani katika sekta ya viwanda.
Mgombea mwenza huyo wa UKAWA Mh. Babu Juma Duni Haji ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akihutubia mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu iliyofanyika katika jimbo la Mtama wilayani Lindi na katika kijiji cha Nanjilinji jimbo la kilwa kusini mkoani Lindi ambapo pamoja na kuwasisitizia wananchi kumchagua mgombea urais kwa tiketi ya Chadema Mh. Edward Lowassa amesema mojawapo ya barabara ambazo serikali ya Chadema na UKAWA itaijenga kwa kiwango cha lami ni barabara ya masasi hadi liwale yenye urefu wa zaidi ya kilometa120 ili iweze kupitika wakati wote wa mwaka.
Makamu mwenyekiti wa Chadema taifa upande wa Zanzibar, Said Issa Mohamed akiwahutubia wananchi wa jimbo la Mtama Lindi vijijini ametoa tahadhari kwa wananchi watakaokwenda kupiga kura siku ya Oktoba 25 mwaka huu, huku mgombea ubunge wa jimbo la Lindi mjini Salum Baruan akilazimika kupanda jukwaani ili kuweka sawa hali ya mambo baada ya wagombea wawili wa jimbo la Mtama, Seleman Mathew maarufu kama messi wa Chadema na Isihaka Rashid Mchinjita wa chama cha wananchi CUF kujikuta wakigombea jimbo moja tofauti na uamuzi wa kamati kuu ya UKAWA wa kuachiana majimbo.
No comments:
Post a Comment