WANACHAMA wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamepandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini wakikabiliwa na mashtaka manane ya shambulio la kudhuru mwili kwa kutumia mawe na kuharibu mali.
Washtakiwa walisomewa mashtaka yao jana na Mwanasheria wa Serikali, Beatrice Nsana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi James Karayemaha. Waliofikishwa mahakamani ni Juma Bika (Mtaalam), George Mwingira, Fulgence Mapunda na Deogratia Peter.
Akisoma mashtaka Beatrice alisema washtakiwa hao walitenda makosa hayo Septemba 11 katika eneo la njia Panda ya Naam Area C mjini hapa.
Mwanasheria huyo aliwataja waliwashambulia ni Fatma Issa, Athuman Waziri, Sira Aron na Christina Mulugu.
Alidai pia washtakiwa hao walifanya uharibifu katika magari manne miongoni mwao moja ni mali ya CCM.
Washtakiwa wote ambao wanatetewa na Wakili Fred Kalonga walikana mashtaka hayo na kupewa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yakiwa ni kuwa na mdhamini mmoja kila mshitakiwa, barua utambulisho ya ofisa mtendaji wa kata na Sh. milioni moja.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 5, 2015 itakapotajwa tena na upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupata dhamana, Mwingira ambaye ni Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji Chadema Taifa amesema kesi hiyo ni mbinu za CCM kuharibu na kuwatisha watanzania wasiendelee na mchakato wa kuhakikisha mgombea wa UKAWA, Edward Lowasa anaingia Ikulu.
“Hatutatishika, tutakwenda mbele kwa mbele hadi tuhakikishe Lowassa anaingia Ikulu,”amesema.
No comments:
Post a Comment