Dar es Salaam. Tangu kuzinduliwa kwa kampeni, hoja ya ufisadi imeonekana kuvigawa vyama vikuu vinavyopambana kwa karibu huku mgombea wa urais wa CCM, Dk John Magufuli akiitumia kama kete muhimu ya kumpatia ushindi na kuwapunguza makali wapinzani wake.
Hoja hiyo iliyokuwa ikitumiwa zaidi na vyama vya upinzani kuwavuta wapiga kura katika uchaguzi uliopita, imegeuka lulu kwa CCM na kuwavutia wananchi wengi kila anapopita Dk Magufuli kuhutubia, huku wapinzani wakionekana kuiweka kando.
Kwa nyakati tofauti, Dk Magufuli amekuwa akiwaomba wananchi wasiichukie CCM na Serikali kwa sababu ya mafisadi wachache ambao huwafananisha na kunguni kwenye kitanda na kwamba akiingia madarakani, atawachoma moto ili kitanda kibaki salama.
Wakati mgombea wa CCM na timu yake ya kampeni wakishikilia kete hiyo, safari hii Chadema na Ukawa pamoja na mgombea wao, Edward Lowassa wameiweka kando kete hiyo na kuchukua ya ‘mabadiliko’, wakisema wameamua kupanua wigo wa hoja kwa kuwa kupambana na ufisadi ni sehemu ya mabadiliko wanayokusudia.
Akizungumza kuhusu Ukawa kutozungumzia ufisadi kama ilivyokuwa mwaka 2010, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema: “Mabadiliko ni pamoja na kuzungumzia mabadiliko katika utendaji wa serikali na watumishi wa umma, yaani kuboresha utendaji kwa maana ya kuondoa rushwa na ufisadi.
“Kwa sasa neno ufisadi halijitokezi sana kwa sababu tumezungumza ufisadi kwa zaidi ya miaka 10 na Watanzania wanaelewa msimamo wetu, tunahitaji kupanua ajenda yetu na hatuwezi tukagombea uchaguzi wa urais kwenye eneo moja tu la ufisadi, lazima tupanue wigo wa masuala yanayowakabili wananchi.”
Lissu alisema Julai mwaka huu, Chadema iliajiri wataalamu kukusanya maoni ya Watanzania kuhusu masuala mbalimbali wanayoyaona ni muhimu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na katika utafiti huo, suala la ufisadi lilipata asilimia tano huku elimu na utawala bora zikipata alama za juu.
“Maana yake ni kwamba ili kushinda uchaguzi, lazima tuibue masuala mengine ambayo Watanzania wanayaona ya muhimu katika maisha yao,” alisema Lissu.
Viongozi mbalimbali wanaombatana na Lowassa katika mikutano yake, nao hujikita zaidi kuzungumzia mfumo wa utawala unaochangia ufisadi na kuwataka Watanzania kuhakikisha wanawachagua.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amekuwa akiongoza timu ya kampeni ya Lowassa kueleza jinsi Serikali ya CCM ilivyoshindwa kuwaletea wananchi maendeleo kwa miaka 54 tangu uhuru.
Sumaye, mara nyingi hueleza ufisadi uliofanyika tangu Lowassa alipojiuzulu mwaka 2008, huku akihoji yalipo majina ya wauza dawa za kulevya na majangili ambayo kwa nyakati tofauti Rais Jakaya Kikwete amenukuliwa akisema kuwa anayo.
Magufuli na ufisadi
Tangu alipoanza kampeni mikoani Agosti, 24, akianzia Katavi hadi mkoani Simiyu, hakuna sehemu ambayo Dk Magufuli na makada wengine wanaomnadi wameacha kujinadi kuwa CCM itapambana na ufisadi na wananchi wasichague mafisadi kwenda Ikulu.
Dk Magufuli amekuwa akiinadi sera hiyo iliyopo kwenye Ilani kwa msisitizo na kueleza kuwa iwapo atachaguliwa Oktoba 25, ataanzisha mahakama maalumu ya kuwahukumu na kuwafunga mafisadi.
“Nimeomba urais ili nikawafunge mafisadi na makufuli yangu na kutokana na misimamo yangu baada ya mimi kuteuliwa wengine wameshaanza kukimbia,” alisema Dk Magufuli hivi karibuni akiwa Nyamongo, Tarime na kushangiliwa.
Mgombea huyo alisema kazi yake kubwa ni kuwamaliza mafisadi na wala rushwa wachache wanaowanyonya wananchi wengi wa kipato cha chini.
Dk Magufuli amekuwa haishii kuhubiri mikakati yake ya kuondoa watafunaji wa fedha za umma tu, bali wakati mwingine amekuwa hata akirusha vijembe vya chinichini upande wa pili wa upinzani kuwa wamepokea ufisadi.
“Hata wakati huu wa kampeni kuna watu wameweza kununua mabasi 30 wamepata wapi fedha kama hawajaiba humuhumu serikalini? Nikipata urais nitawashughulikia wote,” alisema mgombea huyo bila kufafanua.
Huku akieleza kwa mifano, mgombea huyo alisema: “Ukiwa unachunga kondoo halafu mbwa mwitu wakakimbilia kwenye kondoo halafu hao kondoo hawashtuki, utajiulizaje wewe mchungaji, ulikuwa unachunga kondoo au ni mbwa mwitu waliovaa ngozi za kondoo? “ alihoji na kusindikizwa na shangwe za wanakijiji wa Mkamba wilayani Kilombero na kuongeza:
“Kwa hiyo ukiona mtu amekimbilia mahali na alikuwa fisadi maanake na wale wote waliompokea walikuwa mafisadi ila walikuwa wamevaa tu nguo za wema.”
Waziri huyo wa ujenzi amekuwa akisaidiwa na vigogo wengine ndani ya chama hicho kunadi sera ya kuwang’oa mafisadi katika uzito unaofanana huku mara nyingi wakitaka wananchi wasimchague Lowassa wakimtuhumu kwa ufisadi wa Richmond.
Baadhi ya vinara wa kuipiga Ukawa na mgombea huyo, ni mawaziri, Dk Harrison Mwakyembe, Stephen Wasira na Mwigulu Nchemba pamoja na wajumbe wengine wa timu ya kampeni ya CCM.
Kama hiyo haitoshi, makada wa CCM wamekuwa wakitumia nafasi ya kuhama kwa Sumaye kwenda Ukawa, kuukandia upinzani kwa wananchi kuwa nao “wamegeuka mafisadi” baada ya kumpokea kigogo huyo.
Pia, CCM imemwibua aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Yusuph Makamba ambaye aliitumia vizuri mikoa ya Morogoro na Tanga kumnadi Dk Magufuli kuwa ni kiongozi mwadilifu anayefaa kuwa rais na si Lowassa ambaye tangu mwaka 1995 Kamati Kuu ya CCM ilimkataa kwa kuwa “ni kijana mdogo mwenye mali nyingi zisizo na maelezo ya kutosha kuhusu vyanzo vyake.”
Kauli ya wasomi
Akizungumzia hoja hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema suala la kupambana na ufisadi lilikuwa mkakati wa muda mrefu wa CCM.
“Walishajipanga kwa hilo ndiyo maana katibu mkuu wa chama hicho (Abdulrahman Kinana), katika ziara zake alikuwa anakikosoa chama chake,” alisema Mbunda.
Alisema kiongozi huyo na baadhi ya wenza wake, wamekuwa wakisisitiza kwamba wanataka mtu safi na hata mgombea wa urais walishamwandaa.
“Walipanga pia mgombea wao awe kinara wa kuikosoa Serikali na kuahidi kushughulikia masuala ya ufisadi na kwamba hata akiingia madarakani atapambana na ufisadi,” alisema Mbunda.
“Huo ni mkakati wao ili kubaki madarakani. Hakuna chama cha siasa kinachopenda kung’oka madarakani,” alisema.
Profesa Tolly Mbwete alisema suala la ufisadi limekuwa likizungumzwa tangu nyuma: “...Sisi tunataka kusikia mambo ya msingi yenye manufaa kwa wananchi wa Taifa hili. Kuzungumzia matatizo ya wananchi na namna ya kuyatatua… tunataka kusikia hoja za msingi. Tena tunataka kusikia wakitueleza ni wapi watapata fedha za kutelekeza ahadi wanazotoa kwa Watanzania.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sauti ya Mwanamke Tanzania, Laetitia Petro alisema: “Ufisadi ni tatizo ambalo lipo nchi nzima na kwa hali ilivyo sasa hatutegemei Chadema wakazungumzia jambo hilo, lakini hata CCM pia siyo wasafi.”
Wakili huyo wa kujitegemea alisema wanasiasa wanatakiwa kutumia muda wao wa kampeni kunadi sera na namna watakavyotatua matatizo ya wananchi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya AHA, Abbas Said aliunga mkono hoja zilizotolewa na baadhi ya wasomi na kusema kuwa, hizo ni zote ni mbinu za kampeni ili washinde uchaguzi.CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment