Wednesday, December 2, 2015

Zanzibar yapata Meli mpya




MELI mpya ya MV.Mapinduzi ( ii) imewasili bandarini Zanzibar kwa ajili ya kuanza safari zake baada ya kukamilika ujenzi wake huko Korea ya kusini.

Hafla ya kuwasili kwa meli hiyo imeongozwa na waziri wa fedha Omar Yussuf Mzee ambapo amesema ujenzi wa meli hiyo ni agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Amesema meli hiyo bado iko katika mikono ya wajenzi hadi sasa na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi wiki ijayo na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein ambaye ni mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

Waziri mzee amesema meli hiyo inavifaa vya kutosha kama vile life jacket, pamoja na boti ndogo ili kuweka usalama kwa abiria wataosafiri katika meli hiyo.

Hata hivyo amesema meli hiyo itasafiri pemba pamoja na Dare-salam hivyo amewataka wananchi kuitunza meli hiyo kwani ni matunda yao.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano Zanizar Dk. Juma Malik amesema lengo kulifanya shirika la meli lifanye kazi kibiashara ili kuongeza pato la Taifa.

Amewaomba wananchi kuitunza na kuitumia vizuri meli hiyo kwani wamefanya kazi kubwa na kutumia gharama hadi kufikia kukamilika kwa meli hiyo.

Sambamba na hayo amesema meli hiyo ina uwezo wa kupakia abiria wasiopungua 1,200 pamoja na tani za mizigo 200.

Meli hiyo mpya ya MV.Mapinduzi ( ii) imetengenezwa Korea kusini na kugharimu jumla ya dola mil.30.4 za Marekani ambapo ujenzi wake hadi kukamilika umechukua jumla ya miezi 18.

Imetolewa na maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment