Saturday, October 17, 2015

Zinduka 10 - Kuondoka kwa Lowassa Kuliisafisha CCM? Majibu Maridhawa

Ni mwendelezo wa majibu ya hoja dhaifu ambazo zimekuwa zikitolewa kuhalalisha kutumika kwa Lowassa kujaribu kuiondoa CCM. Hoja kuwa kuondoka kwa Lowassa hakukuifanya CCM kuwa safi kwani ufisadi umeendelea kuwepo licha ya yeye kuondoka Serikalini miaka nane iliyopita; hii nayo ni hoja muflisi kama nitakavyoionesha na inasikitisha inapotolewa na watu ambao wanaonesha dalili ya umakini katika ujengaji hoja ila kwa kile ambacho wenyewe leo wanakiita "mahaba" basi wamepoteza hata umakini katika ujengaji hoja. 



KUPANGULIWA KWA HOJA DHAIFU – 2 “Kuondoka kwa Lowassa Kumeisafisha CCM; Ufisadi Aliondoka Nao?

Na. M. M. Mwanakijiji
Kama nilivyoonesha jana, watu wengi ambao wamejitokeza kuwa wanamtaka Lowassa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wamekuwa wakitoa hoja nyingi dhaifu na muflisi ukizisikia tu. Zinatolewa hoja na baadhi ya watu ambao unajua kabisa wangetulia chini wangeweza kuona ubovu (fallacy) ya hoja zao kwani zimefikiriwa upande mmoja tu bila kuangala kina chake. Leo ni mwendelezo wa kupangua hoja hizi ili kuhakikisha kuwa kila mtu anayenda kupiga kura awe anajua kabisa anapiga kura kwanini. Mtu anayepiga kura bila sababu ya makini huweza kupiga kura itakayomkata maini mbeleni!

Mimi ni M. M. Mwanakijiji – Operesheni Zinduka 10

Katika makala ya jana nilipangua hoja kama nne tu na kuonesha ni jinsi gani zimethibitisha maneno ya Mch. Msigwa Bungeni kuwa wakati mwingine tunaacha akili ndogo zitawale akili kubwa. Kwamba, kama alivyosema – na ninakubaliana naye kabisa – kuwa matatizo hayawezi kuondolewa na upeo ule ule wa fikra ambao uliyasababisha. Hii ndio sababu wengi wetu tuliamini kuwa CHADEMA ilikuwa imejipanga vizuri mwaka huu kuleta upeo mpya wa fikra ambao utakabaliana na matatizo yetu.

Nilionesha katika makala ile – ambayo hatukuwa tumetengeneza video na sasa tumetengeneza – kuwa hoja zzote ni muflisi. Leo nataka niendeleze kupangua hoja kubwa mbili – zisizohusiana ukiondoa tu kuwa zote zinahusiana na uongozi. Ya kwanza, ni hoja ambayo tumeidokeza kwa mbali huko nyuma lakini inahitaji kuangalia kwa karibu.

1. Mbowe ni Kiongozi Mzuri Aliyeweza Kubadilisha Gia Angani

Kinyume na imani hi ambayo baadhi ya watu (hasa waliodandia kutoka CCM kuja CDM na Lowassa) Uamuzi wa CHADEMA kumtegemea Lowassa kuiongoza ushindi ni ushahidi tu kuwa Mbowe amejionesha kwa bahati mbaya sana kushindwa uongozi. Kwa miaka karibu mitano, Mbowe kama Mwenyekiti aliwaaminisha Watanzania kuwa chama chake kilikuwa tayari kuchukua dola; ukweli ni kuwa yeye mwenyewe hakuwa anaamini kuwa wana watu wanaweza kushika nafasi ya Urais na wakakubalika.

Tukikubaliana – kwa ajili ya hoja yetu hii leo – kuwa Dr. Slaa hakuwa na kuweza kushinda dhidi ya mgombea yeyote wa CCM swali kubwa ambalo lilipaswa kuulizwa na wanachadema na wote waliounga mkono ni je hakukuwa na mtu mwingine yeyote ndani ya chama hicho ambaye angeweza kwenda sambamba na mgombea yeyote wa CCM. Mbowe mwenyewe bila ya shaka hakuwa na uwezo huo (alisharibu na kushindwa mara moja!); vipi kuhusu Profesa Safari, vipi kuhusu Profesa Baregu, vipi kuhusu watu wengine mbalimbali maarufu wa CDM? Yaani, kati ya watu wote hakukuwa na mtu mwingine yeyote mwenye uwezo wa kuwa Rais ndani ya CDM ukiondoa Dr. Slaa? Hata Tundu Lissu hakuwa na uwezo wa kuwa Rais wakati alionekana ni mtu ambaye naye anakubalika (kama ukipima kwa umahiri wakuongea Bungeni na kuichachafya serikali?

Jibu ni rahisi kuliona – hakukuwa na mtu mwingine yeyote ambaye Mbowe na Kamati Kuu aliyoingoza angeweza kusimama kushindana na CCM. Hili ni jambo la fedheha, kejeli, na kufuru kwa demokrasia! Yaani, miaka yote ile kumbe wenzetu walikuwa hawana watu wa kushika nafasi ya Urais?

Hivi, tunaweza kuamini wana watu wa kushika nafasi yoyote ya Uwaziri? Siyo kwamba ujio wa kundi kubwa la wana CCM ambao wamewahi kushika nafasi mbalimbali ni dalili tu kuwa Mbowe na viongozi wenzake (kama tunaweza kuwaita hivyo kweli) wameona kuwa hawana hata watu wenye uwezo wa kushika Uwaziri na badala yake wamewapigia mahesabu kina Masha, Mgana Msindai, Sumaye, Kingunge n.k? Yaani, siyo tu wana CCM waliangaliwa kuja kutoa Rais wa CHADEMA hata mawaziri wanaangaliwa kutoka CCM?

Lakini wale wanaotoka CCM siyo watu ambao unaweza hata kusema unafurahia kuwachukua; ni watu ambao tayari wameonesha kushindwa CCM leo wamekumbatiwa CHADEMA? Isije kuwa wale watu maarufu wa CDM ambao tuliamini ni potential leader materials wote wanasubiri vijinafasi vya Ukuu wa Mkoa na Ukuu wa Wilaya!?
Hii ni fedheha ya kiuongozi na lawama zote zinamuangukia mtu mmoja tu – Freeman Mbowe. Miaka yote hii ya kujionesha kuwa ni kiongozi kumbe hakuandaa mtu hata mmoja wa kuweza kushika Urais au Uwaziri!

2. Hoja ya pili ndio imebeba kichwa cha habari hapa; na hoja hii imetolewa na baadhi ya watu ambao wengine ninawaheshimu kweli kweli kwa uwezo wa kutoa hoja. NImetumiwa na baadhi ya watu hoja hii kunionesha makosa ya hoja yangu na ndio maana nataka niijibu. Hoja hii ni moja ila ina pande mbili.
Upande wa kwanza inauliza kama kuondoka kwa Lowassa kumeisafisha CCM? Na upande wa pili mbona pamoja na kuondoka Serikalini miaka nane iliyopita bado ufisadi umeendelea? Hoja hii ukiiangalia unaweza kuifurahia lakini ina makosa makubwa kadhaa na ambayo mtaalamu wa ujengaji hoja kama mimi naweza kuyaona hata kabla hayajakamilika!

Kwanza, hakuna shaka hata kidogo kuondoka kwa Lowassa ni nafuu kwa CCM. Hili siyo suala la usafi tena hasa kwa sababu wanaotoa hoja ya usafi ndio wale wale wanaosema “hakuna mtu msafi, wote tuna makosa”. Kama hakuna mtu msafi na wote tuna makosa basi bila ya shaka ni lazima tujiulize nani msafi zaidi.

Kuna msemo kuwa “kuvuja kwa pakacha ni nafuu kwa mchukuzi”. Msemo huu una ukweli fulani. Lowassa alikuwa ni tatizo (enigma) ndani ya CCM. Aliisumbua CCM na alionekana kuilazimisha impe nafasi ya kugombea vinginevyo ingekuwa mbinde. Aliwathubutisha na kuonekana kama ameishikia kisu Kamati Kuu imkate jina lake ione. Lakini hakuanzia hapo tu; aliisumbua CCM kiasi cha kusababisha yeye na wenzake kupewa maonyo n ahata kufungiwa kwa muda. Hakujifunza lolote kwani Lowassa siyo mtu wa kusimamiwa na mtu yeyote.

Sasa kuondoka kwake na wale ambao walikuwa wanamuunga mkono hakuwezi kuwa jambo baya kwa CCM! CCM inashukuru kwamba haiangaiki na Lowassa na tunaoweza kuwaita mamluki wake (angalau siyo wale waliobakia kwa siri).

Hata mtu akianza kupata nafuu kutoka ugonjwa fulani kwake ni heri kuliko kuendelea kuugua ugonjwa na kulala kitandani. Lowassa kuondoka hakujaisafisha CCM lakini hakujaichafua! Na tunaweza kusema kwenda mbali na kusema kumeipa CCM ahueni kiasi kwamba kama ilikuwa inapumua kwa shida sasa angalau imeanza kupumua. Na imepumua kwa sababu nyingine kuwa hakuondoka kwenda kwingine bali kule kuliko kunaisababishia homa CCM! Sasa kwanini CCM isishukuru Mungu? Kwanini CCM isijione ina nafuu wakati ni kweli?

UPande wa pili wa hoja hii na ambao unahusiana hasa na uongozi ni kuwa mbona ufisadi umeendelea hata Lowassa kuondoka serikalini? Swali hili linaulizwa kimtego? Utaona watu hawaulizi Mbona ufisadi umeendelea licha ya Lowassa kutoka CCM na kujiuzulu Ubunge? Ukweli ni kuwa Lowassa alitoka serikalini tu lakini alikuwa badoni mwanachama mwaminifu wa CCM na kiongozi ndani ya chama hicho. Alikuwa ni miongoni mwa viongozi ndani ya Bunge (akiwa Mwenyekiti wa Kamati Mbili tofauti wakati tofauti).

Sasa ni lazima tuelewe kuwa kazi ya kiongozi ni kuongoza siyo kufuata! Lowassa alipoamua kubwaga manyanga kufuatia Kashfa ya Richmond hakuzuri tu Uwaziri Mkuu alizira yna Uongozi! Angekuwa ni kiongozi mzuri angesimama kupigania mambo aliyoyaamini – elimu, huduma bora n.k. Angekuwa ni kiongozi mzuri angeleta hata miswada ya kuinua ajira badala ya kuwananga wenzie ati kwa kushindwa kuchukua maamuzi magumu! Angekuwa ni kiongozi mzuri kivile angepinga uvunjwaji wa haki za binadamu uliofanywa na vyombo ambavyo alikuwa anavisimamia kwa niaba ya Watanzania kule Bungeni! Lowassa hakuwahi (angalau hadharani na niko tayari kusahihishwa) kukionya chama chake, mawaziri wake, au vyombo vya serikali kwa mauaji ya wananchi wasio na hatia? Hata kwenye sakata la Tokomeza Lowassa hakuonesha uongozi wowote kuonesha kujali wananchi?

Leo hii anazungumzia kuwa ati yeye atakula sahani moja na mama ntilie na wafanyabiashara wadogo na madereva wa boda boda, hivi ni lini alikuja na suluhisho lolote la kuinua maisha yao? Zitto Kabwe pamoja na matatizo yote aliyokuwa nayo CDM lakini aliongoza; si alienda kujitahidi kuwaandikisha vijana kuingia kwenye mafao ya NSSF na mifuko mingine? Lowassa alifanya nini?

Kwa ufupi ni kuwa Lowassa hakuwa kiongozi na kama angekuwa kiongozi basi tungeona akionesha umahiri wake wa kupigana na ufisadi ulikuwepo serikalini. Hivi watu wamesahau kuwa kulikuwa na ripoti karibu sana za CAG ambazo Lowassa angeweza kutoa maoni yake na kuonesha kukasirishwa na ufisadi serikalini kama walivyofanya wabunge wengine? Leo tunaambiwa ati atashughulikia matatizo mbalimbali na wapo watu wanaamini?

Tunaposema Lowassa ni kiongozi mbovu hatumsingizii; tuna ushahidi wala hatuhitaji kwenda mahakamani kuonesha hili. Na Wiki ijayo, nitaonesha kwa mara moja na kufunga kabisa mjadala wa jaribio la Lowassa kukwepa kashfa ya Richmond! Huwezi kutenganisha uongozi wa Lowassa na ujio wa Richmond na matokeo yake. Huwezi. Kila anayejaribu amefeli akiwemo yeye mwenyewe!

Inshallah!

No comments:

Post a Comment