Thursday, October 8, 2015

Operesheni Zinduka -3 : Kamari ya Mbowe na Lowassa Yaweza Kulipa Kweli?

Tunaendelea na operesheni hii na tayari tumeona watu wameanza kufunguka... NB: Kama umeshaamua kumpigia kura Lowassa bila kujali factors nyingine zozote ni vizuri usithubutu kusikiliza shows hizi... utaishia kutukana, kuita watu majina... au kubadili mawazo!







Na. M. M. Mwanakijiji
Mojawapo ya mikakati ya kisiasa ambayo inaweza kuamua kabisa ni kwa kiasi gani harakati za mabadiliko Tanzania zimepata madhara makubwa ni ule uamuzi wa Team Mbowe kuunganisha nguvu na Team Lowassa ili kujaribu kuiondoa CCM madarakani. Mkakati huu inaonekana ulipangwa kwa kiasi kikubwa na kwa usiri mkubwa ili kuhakikisha kuwa vyovyote inavyokuwa Lowassa anapata jukwaa la kujaribu kutimizia ndoto yake ya kuutaka Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa mbinde au kwa upinde katika Uchaguzi huu Mkuu.

Ni vizuri katika episode hii ya leo kuelewa vizuri hesabu za kamari hii na kwanini baadhi yetu tunaamini kuwa ni mojawapo ya mikakati mibovu kabisa ya kisiasa kuweza kubuniwa hasa kwa chama ambacho tayari kilikuwa tayari kushinda. Tunaamini kabisa kuwa hata bila Lowassa CHADEMA ilikuwa na nafasi kubwa na nzuri zaidi ya kuing’oa CCM madarakani na bado ikabakia na sura yake kama chama chenye kutaka na kusimamia uadilifu, utawala bora, maono bora kwa taifa na uongozi bora.

Kamari hii ya kisiasa yaani ‘political gamble’ imeweka hatima za Mbowe na Lowassa kisiasa na hata kiuongozi kwenye sanduku la kura ifikapo Oktoba 25.

Baada ya kumpitisha Dr. Slaa kuwa mgombea wake wa Urais mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2010 CHADEMA ilikuwa inaweka mkazo tu katika mikakati ya kampeni, kupanga wagombea wake katika majimbo na halmashauri mbalimbali ili kuhakikisha kuwa inatoa ushindani wa uhakika dhidi ya CCM. Kama nilivyoonesha jana, uamuzi huu haukuwa mgeni kwani ulitarajiwa na wengi – ndani ya CHADEMA nan je ya CHADEMA. Hii haikuwa kamari ulikuwa ni uamuzi wa kujijua.

Hata hivyo inaonekana CHADEMA haikuwa ina uhakika kuwa imejipanga vya kutosha kiasi kwamba macho yao – hasa baadhi ya viongozi wa Taifa – yalikuwa bado ndani ya CCM wakisubiria nani atoswe ili apewe nafasi kwao. Ni kama ilivyokuwa mwaka 2010 kwa mkakati huu huu ambapo walitarajiwa watu kama Samwel Sitta wajiunge na CHADEMA ili CHADEMA ijipatie mgombea wake wa Urais. Kama ilivyokuwa 2010 imerudiwa tena 2015 kwamba CHADEMA haikujiamini kuwa ina mtu anayekubalika, mwenye msimamo na anayetoka ndani ya chama kuweza kuiondoa CCM madarakani.

Kimsingi pamoja na maandamano yote ya miaka mitano, pamoja na vipigo vyote dhidi yao, pamoja na damu yote iliyomwagika kusimama na CHADEMA na pamoja na watu wote ambao waliamua kujitoa muhanga kuinadi CDM kama chama kinachoweza kuitoa CCM madarakani mwisho wa siku viongozi wakuu wa kitaifa hawakuamini kuwa kwanza, wana watu wenye uwezo na ujiko wa kuweza kushindana na yeyote CCM na pili wana ujumbe wa kuweza kuwafanya WAtanzania wakubali mgombea au wagombea wao. Matokeo yake ni macho yao yalikuwa CCM.

Walisubiri

Waliombea

Walinuia

Waliongea na mwisho walisogelea CCM ili iwapatie mgombea wao wa Urais. Kwamba, ukiondoa Dr. Slaa chama kizima cha CDM hakikuwa na mwanasiasa mwingine yeyote mwenye uwezo, nia, na uthubutu wa kubeba bendera ya CDM kuelekea Uchaguzi Mkuu. Mtu huyo alisubiriwa kutoka CCM na tunavyojua sasa mtu huyo alikuwa mmoja tu Lowassa.

Inawezekana basi – na uwezekano huu ni vigumu kuupinga kwa hoja – mada zote na mazungumzo yote yaliyofanywa na viongozi kama Mbowe, Lissu, Mnyika na wengine juu ya kuhusisha ufisadi na uongozi wa Lowassa yalikuwa ni geresha tu ya kumchagua ili CCM imkate ili wao wampate! Kwamba, yote yaliyokuwa yakisemwa juu ya Lowassa na kuitwa “ushahidi” yalikuwa ni ulaghai usio kifani uliokuwa na lengo la kumfanya Lowassa asiaminike na asikubalike na wenzake CCM chama ambacho kilimlea na kumjenga kisiasa ili hatimaye aje upande huu.

Ukweli huu si mgumu kueleweka hasa kwa vile inaonekana upo ushahidi usio na shaka kuwa mazungumzo kati ya Mbowe na Lowassa ya kumtengenezea sebule CHADEMA yalikuwa yakifanyika kwa usiri mkubwa tangu 2011. Kufa kwa tembo ikawa furaha kwa wanyama wengine porini; kukatwa kwa Lowassa kukawa neema kwa CDM kwamba hatimaye mtu ambaye waliamini anaweza na anafaa kuwaongoza kuiondoa CCM atakuja kwao.

Hapa ndipo kamari ikachezwa Dr. Slaa akakatwa (hili nitalielezea katika show ya Ijumaa jinsi gani Mbowe alimzunguka Slaa ili kumleta Lowassa kinyume na gumzo kuwa Slaa ndiye aliyemleta Lowassa CHADEMA – USIKOSE.

Kamari hii hata hivyo ilifanya makosa makubwa mawili ambayo kwa hakika yatamnyika Lowassa ushindi, kuleta mgogoro mkubwa CHADEMA na washirika wake na hatimaye kufunika hatima za kisiasa za Mbowe na kundi la wale walioungana naye kumleta Lowassa nyumbani.

Kosa la kwanza, ni kuwa walitegemea kuwa ujio wa Lowassa ungeigawa CCM pande mbili na kuidhoofisha. Badala yake CCM haikumeguka kama ilivyotarajiwa. Hadi hivi sasa hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliyeondoka kwenda CDM ambaye alikuwa bado na nafasi CCM! Kuanzia Kingunge na wengine wote ambao hadi hivi sasa wanasema wamejitoa CCM kumfuata Lowassa ambao CCM bado ilikuwa inawaamini kuwa ni makada wake wazuri na wakuigwa. Na hakuna mamilioni ya wanachama wa CCM ambao wamemfuata Lowassa. Hata ahadi mbalimbali za kundi la wabunge sijui kundi la vigogo kuhama hazijatokea na nina uhakika hazitatokea kwa sababu hao watu ni wanasiasa na wao wameshapiga hesabu zao vizuri kwani wameona treni kweli limeondoka stesheni lakini haliendi popote na meli inayosifiwa kuwa imeondoka kumbe imebeba mizigo mingi kiasi kwamba itazama tu.

Kosa la pili na kubwa zaidi ni kuwa uchaguzi hu CHADEMA ingeweza kuiondoa CCM madarakani kirahisi, kwa hoja na kwa mkakati mzuri kama uchaguzi ungehusisha wagombea watatu maarufu. Baadhi yetu tuliamini huu ndio ulikuwa mkakati mzuri zaidi. Kwamba, tulijua Lowassa atagombea tu hata akikatwa CCM hili halikuwa na shaka. Tuliamini pia kuwa (au zaidi tuliaminishwa) Slaa atakuwa ni mgombea wa CDM na kuwa CCM bado ingekuwa na mgombea wake mwingine (sema huyu huyu Magufuli). Hivyo kura za Watanzania zingepigwa vizuri.

Ana kutaka kuendelea na utawala wa CCM iliyomeguka chini ya mgombea Magufuli (au mwingine yeyote) au kumfuata Lowassa alipo na kundi la watu kama milioni moja wenye kumuamini au kumfuata kiongozi ambaye tayari amejionesha ni mwanameguezi wa kweli, na ambaye ameshalipa gharama kubwa ya kukiandaa chama na uchaguzi huu mkuu. CHADEMA isingekuwa imegawanyika ingekuwa moja, ingepata kura za wananchi ambao tayari wanaiunga mkono n ahata wana CCM ambao hawakuwa tayari kuendelea na CCM wala kumfuata Lowassa aliko.

Siri ya hili iko kwenye kuelewa kuwa mshindi wa kura ya Urais anatakiwa apate “kura nyingi” (kwa mujibu wa Katiba yetu Ibara 41.6 tu kutangazwa mshindi. Katika uchaguzi wa pande tatu ambao wengi tuliutarajia mgombea wa CCM na Lowassa wangegawana angalau asilimia sitini kati yao wakati mgombea wa CHADEMA angeweza kushinda hata kwa asilimia 40 ya kura. Na hata kama ingekuwa kwa asilimia 50 + 1 bado mgombea wa CDM angeweza kupigigania kupata asilimia hizo hasa tukizingatia kuwa mwaka 2010 Dr. Slaa alishusha kura za Kikwete toka asilimia 80 za 2005 hadi kama asilimia 62 hivi. Uwezekano wa mgombea wa CCM iliyogawanyika kupata kura chini ya hizo kimehasabu ulikuwa mkubwa zaidi katika mbio za wagombea watatu wakubwa.

Hata hivyo, kamari hii imesababisha kura ziwe za pande mbili; Magufuli upande mmoja na Lowassa upande mwingine. Mbio hizi sasa siyo tena za taasisi mbili (kama nilivyoonesha jana); ni mbio za watu wawili tu – Lowassa upande mmoja na Magufuli upande mwingine. Upande mmoja ni Magufuli na taasisi ya CCM na mifumo yake yote na upande mwingine Lowassa – peke yake; hana taasisi – akitegemea nguvu ya jina lake tu wala siyo historia yake au maono yake kama kiongozi wa upinzani.

Ni vigumu kuona ni jinsi gani Lowassa anashinda ati kwa vile watu wanataka tu ashinde au wanaamini watu wameichoka CCM! CCM hii ambayo sasa inaonekana imepewa uhai mpya kwa kuondokewa na watu wake waliokuwa matata sana ina nafasi kubwa zaidi ya kushinda kuliko CDM ambayo ilijivuruga yenyewe kw akutafuta njia ya mkato kutaka ushindi.

Kamari haitalipa; Lowassa atagaragazwa na kuvuruga kwa muda mrefu ujao harakati za mabadiliko ambazo nusura zingezaa matunda mwaka huu.

Ilikuwaje Lowassa akaingia CDM hata hivyo? Tukutane kesho!

No comments:

Post a Comment