Monday, October 12, 2015

Makala ya BBC: Mfahamu Magufuli mgombea urais wa CCM

Magufuli2

John Pombe Magufuli, mgombea urais kupita Chama cha Mapinduzi, kitaaluma ni mwalimu na mtalaamu wa Kemia.
Alizaliwa Oktoba 29 mwaka 1959 huko Chato mkoani Kagera, Kaskazini magharibi mwa Tanzania.


Magufuli alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi huko huko Chato, mkoani Kagera kuanzia mwaka 1967 hadi 1975 na baadaye akajiunga na shule ya sekondari ya Lake iliyoko Mwanza mwaka 1977 hadi 1978.

Kiongozi huyo alijiunga na chuo cha ualimu cha Mkwawa kilichoko Iringa, Kusini mashariki mwa Tanzania kati ya mwaka 1979 na 1982 ambapo alitunukiwa Stahahada ya Ualimu. 
Baada ya kufuzu, alifundisha masomo ya hisabati na kemia katika shule mbalimbali za sekondari kuanzia mwaka 1983.
Magufuli hakuishia hapo kielemu kwani aliamua kujiendeleza zaidi na kujiunga na chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1985 hadi 1988 ambapo alitunukiwa shahada ya ualimu katika masomo ya kemia na hisabati.
Baadaye, aliamua kukolea katika kemia na akarejea chuoni na kusoma hadi ngazi ya udaktari.

Siasa za Tanzania

Katika siasa za Tanzania, Magufuli mwanzoni hakujulikana sana, hadi nyota yake ya kisiasa ilipoanza kung’aa pale alipogombea na kushinda ubunge eneo la Chato mwaka 1995.
Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye akapanda ngazi hadi kuwa waziri kamili, nafasi aliyoishikilia hadi hivi sasa.
Kwa mujibu wa majirani wanaoishi karibu na nyumba yake jijini Dar es Salaam, yeye ni mtu anayeishi maisha ya kawaida.
Wakati watoto wa baadhi ya viongozi wakisoma shule za hali ya juu watoto wake wamesoma katika shule za kawaida.
Tofauti na uchaguzi uliopita ambapo chama cha CCM hakikukabiliwa na upinzani mkali, Magufuli anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mgombea wa upinzani Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa.
Bw Lowassa anagombea kupitia chama cha upinzani cha CHADEMA, akiwakilisha muungano usio rasmi wa vyama vinne vya upinzani unaojulikana UKAWA.

Elimu

2006 – 2009: PhD (Kemia ); Chuo Kikuu cha Dar es salaam
1991 – 1994: Msc. (Kemia); Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Tanzania na Chuo Kikuu cha Salford, Uingereza
1985 – 1988: Shahada ya kwanza katika Ualimu (Kemia na Hisabati);Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
1981 – 1982: Diploma ya Ualimu masomo ya Sayansi; Chuo cha Ualimu cha Mkwawa Masomo makuu Kemia, Hisabati na Ualimu.
1979 – 1981: Kidato cha tano na sita, Shule ya Upili ya Mkwawa, Iringa
1977 – 1978: Elimu ya sekondari, Shule ya upili ya Lake, Mwanza
1975 – 1977: Katoke Seminary, Biharamulo, Kagera
1967 – 1974: Shule ya Msingi, Shule ya Msingi Chato – Kagera

Mafunzo ya kijeshi

Machi 1984 – Juni 1984: Jeshi la Kujenga Taifa Mpwapwa – Dodoma
Januari 1984 – Machi 1984: Jeshi la Kujenga Taifa Makuyuni– Arusha
Julai 1983 – Desemba 1983: Jeshi la Kujenga Taifa Makutupora – Dodoma.

No comments:

Post a Comment