Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai ambaye ametoa tathmini hiyo mapema jana kwa waandishi wa Habari visiwani humo.
Na Faki Mjaka
[MAELEZO-ZANZIBAR]. Chama cha Mapinduzi CCM kimetoa tathmini yake ya mwelekeo wa Kampeni za Uchaguzi mkuu zinazoelendelea nchini na kudai kuwa Mgombea wake wa Urais Dkt Ali Mohamed Shein anakubalika kwa zaidi ya Asilimia 60 dhidi ya Wagombea wengine.
Akitoa tathmini hiyo mbele ya Wanahabari Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai amesema hatua hiyo ni ishara ya ushindi mkubwa kwa CCM kuliko chaguzi zote toka kuasisiwa kwa mfumo wa Vyama vingi nchini.
Vuai amesema kuna mambo mengi ambayo yamemfanya Dkt Shein kukubalika kwa Wananchi ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-15 kwa zaidi ya asilimia 90.
Amesema katika kipindi chake cha uongozi mgombea huyo ameimarisha uchumi kutoka asilimia 6.0 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2014 na kuongeza kasi ya maendeleo.
Aidha Vuai amefahamisha kuwa udhaifu mkubwa wa Mgombea wa Chama kikuu cha upinzani ambaye ameshiriki chaguzi mara nne bila kufanikiwa nayo ni miongoni mwa sababu zinazokipa ushindi CCM.
Ameongeza kuwa Kampeni zimezidi kupata mafanikio kutokana na mashirikiano ya karibu na Vyombo vya habari na Mitandao ya Kijamii kama vile Facebook, Youtube na Website ambapo huweka Taarifa mbalimbali na Makala zinazohusu maendelea ya Mgombea huyo.
Akielezea changamotoa walizokumbana nazo katika Kampeni ni pamoja na kushambuliwa na kujeruhiwa kwa Wafuasi wa CCM walipokuwa wakibandika Picha za wagombea maeneo ya Darajani mjini Zanzibar.
Aidha amedai kuwa kuna Chama kimoja cha upinzani kimejiandaa kufanya fujo siku ya uchanguzi ili kuharibu zoezi la uchaguzi na kwamba bado wanafuatilia kwa karibu taarifa hizo ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.
Hata hivyo Naibu huyo wa CCM Zanzibar amesema CCM itaendelea na kampeni zake za kistaarabu na kwenda kuomba kura kila kona kwa lengo la kumfikia kila mpiga kura.
Hii ni mara ya kwanza kwa Chama hicho kutoa tathini ya Mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu unaokuja ambapo Naibu Vuai amedai kuwa dalili za ushindi wa kishindo zinaonekana wazi wazi kwa Chama hicho hasa kutokana na mashirikiano mazuri ya Wananchi wa Pemba.
No comments:
Post a Comment