Operesheni Zinduka: Ilikuwaje Dr. Slaa “Amlete” Lowassa CHADEMA Halafu aje kumruka?

Na. M. M. Mwanakijiji

Mojawapo ya maswali ambayo yamesumbua vichwa, kuacha vinywa wazi na kuhoji ukweli au hata nia na uadilifu wa Dr. Slaa katika ujio wa Lowassa CHADEMA ni taarifa kuwa ni Dr. Slaa aliyemleta Lowassa kwa Kamati Kuu baada ya posa kuletwa na aliyemuita “mshenga” Askofu Gwajima. Ilikuwa kuwaje hili? Kama kweli Dr. Slaa hakumtaka Lowassa CHADEMA ilikuwaje akawa wa “kwanza” kumleta”? Swali hili linapatiwa jibu litakalomshtua kila mwenye kuamini simulizi hili – akiwemo Dr. Slaa mwenyewe!

(simulizi la Slaa hapa – video/audio)

Swali hili kama lilivyo hapo linaonekana ni sahihi na linaacha jibu moja tu nalo ni kuwa Dr. Slaa aliamua kumtosa Lowassa kwa sababu yeye alikatwa kugombea Urais na nafasi yake kupewa Lowassa. Je hivyo ndivyo ilivyo? Au kuna kitu kingine cha kutisha zaidi na chenye kuonesha usaliti uliopitiliza katika ujio huu wa Lowassa? Je, swali lenyewe hili lilivyo ni sahihi?

Ili kujibu maswali haya na mengine yatokanayo hatuna budi kurudi nyuma zaidi ya sakata hili; kurudi nyuma na kuangalia baadhi ya matuko ambayo yatatoa jibu lenye kueleweka na ambalo litawazindua wengi hasa ambao wanaamini kuwa ujio wa Lowassa ni jambo lililotokea kwa nasibu tu au kuwa ni “mpango wa Mungu” kama baadhi yao wanavyodai.

Inabidi turudi nyuma kidogo hadi mwaka 2010 na hata ikibidi kurudi nyuma hadi mwaka 2005. Na katika pande hizi zote tunakutana na jina moja ambalo tutakuja kukutana nalo tena mwaka 2015 – Freeman Aikeli Mbowe maarufu kama Kamanda wa Anga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA.

Mwaka 2005 katika nafasi ya kugombea Urais Freeman Mbowe alijaribu bahati yake dhidi ya wagombea wengine maarufu akiwemo Prof. Lipumba na Jakaya Kikwete kutoka vyama vikuu vya siasa nchini wakati huo. Katika uchaguzi ule uliofanyika Disemba 14, 2005 badala ya Oktoba 30 kama ilivyopangwa kufuatia kifo cha Mgombea Mwenza wa CHADEMA Mbowe alishika nafasi ya tatu nyuma ya Lipumba na Kikwete. Kikwete akiwa na kura zaidi ya milioni tisa, wakati Lipumba akiwa na kura karibu milioni moja na nusu hivi. Mbowe alikataliwa na Watanzania kupewa nafasi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Alipata kura karibu laki sita hivi na nusu. CHADEMA bila ya shaka hakikuwa chama chenye nguvu iliyokuwa nayo miaka mitano baadaye.

Baada ya kuibuliwa kwa kashfa mbalimbali za ufisadi kati ya 2005-2010, kinara wa vita hiyo alikuwa ni Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr. Slaa ambaye alikuwa amejipatia umaarufu mkubwa sana nchi nzima. Umaarufu ule ulifanya Mbowe na wenzake wajaribu kupiga mahesabu ya kisiasa ya jinsi gani wanaweza kuikaribia zaidi Ikulu kuliko 2005. Kama nilivyoonesha jana wote (akiwemo Slaa) walionekana kuombea mchafuano ndani ya CCM ungewapatia mgombea mzuri – hili halikutokea na dakika za mwisho Dr. Slaa akaombwa na chama chake kuacha kugombea Ubunge ili agombee Urais.

Katika hili Mbowe aliamini kuwa mwamko wa mabadiliko kisiasa hata kama ungewanyima Ikulu ungetoa nafasi kwa CDM kuwa na wabunge wengi zaidi kuliko CCM na hivyo kuweza kumtoa Waziri Mkuu ambaye kwa hesabu zake – zilizokuwa zinajulikana kwa watu wa karibu wakati ule ni kuwa yeye angepewa Uwaziri Mkuu kwenye Bunge lenye wabunge wengi wa CHADEMA.

Matokeo ya Uchaguzi hayakuwa hivyo sana; CHADEMA haikuchukua viti vingi zaidi Bungeni lakini Dr. Slaa akishindana na Kikwete na Lipumba tena. Safari hii CHADEMA ikinadaiwa na Katibu Mkuu wake ilishika nafasi ya pili lakini kwa kishindio kikubwa kuliko ushindi wa Kikwete mwenyewe. Kura za Kikwete zilishuka toka milioni tisa za 2005 hadi kura milioni tano tu hivi (karibu nusu ya alizopata 2005) wakati Lipumba zilishuka kwa zaidi ya theluthi mbili hadi kama laki saba hivi wakati zile za CHADEMA chini ya Slaa zilipanda hadi milioni 2.2.

Kwa Mbowe hata hivyo nafasi ya Ikulu ilikuwa bado mbali. Mwaka 2015 hesabu nyingine Mbowe alizipiga za jinsi gani anaweza kuisogeza zaidi CHADEMA karibu na Ikulu lakini kinyume na watu wengi wanavyofikiria ni hesabu za jinsi gani yeye anaweza kukaribia zaidi kiti cha Uwaziri Mkuu ambacho alikikosa 2010 na kuishia kuwa kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB).

Hapa ndipo mkakati wake ulipoanza tangu 2011. Taarifa za uhakika na zisizo na shaka zinaonesha sasa kuwa Mbowe na Lowassa (wakitumia wapambe wao muhimu zaidi) walianza mazungumzo ya kumtengeneza njia Lowassa kwa usiri mkubwa huku akimzunguka Katibu wake Mkuu Dr. Slaa. Mbowe aliamini na aliweza kuwashawishi baadhi ya watu ndani ya Kamati Kuu (ushahidi ni watu kama wawili tu) ambao walikuwa wanajua hili kuwa Dr. Slaa asingeweza kushinda Urais mwaka huu.

Mbele ya Dr Slaa Mbowe na wenzake hawa waliendelea kumuaminisha kuwa yeye ndiye mgombea wao na watasimama naye. Ulikuwa ni ulaghai wa kisiasa kwani Slaa kwao alikuwa siyo Plan A bali alikuwa ni kuwa Plan B. Plan A ya Mbowe ilikuwa ni Lowassa. Makubaliano yao yalikuwa tayari yako yameshatengenezwa na kilichosubiriwa ilikuwa ni Lowassa akatwe CCM ili ile hatua ya kumleta CHADEMA ifanyike.

Ushahidi wa hili unaonesha pasi ya shaka kuwa Mbowe alijua kwa uhakika wa kutosha kabisa asingeweza kumleta Lowassa CHADEMA na hakuna mtu mwingine yeyote ambaye angeweza kumleta bila kusababisha shuku. Kulikuwa na mtu mmoja tu mwenye kuaminika, mwenye kukubalika na mwenye ujiko wa kuweza kukaa na Lowassa na kumsikiliza na kumleta mbele ya wajumbe. Huyu ni Dr. Slaa.

Katika zile wiki mbili za “Ukimya” – picha ya kuwa Lowassa anaombwa na kufuatwa na viongozi wa CHADEMA kumshawishi aingie CHADEMA ikaanza kutengenezwa. Ambao hawakukijua ni kuwa picha ilikuwa imeshatengenezwa hawa wengine walikuwa wanatengeneza frame tu ya kuweka picha hiyo.

Ndipo Mshenga – Gwajima - huyu alikuwa ni miongoni mwa watu wachache waliokuwa wanajua mpango wa Mbowe na Lowassa karibu mwaka mmoja kabla. Alikuwa ni mtu anayeaminika na familia ya Slaa na kutokana na cheo chake cha kidini alionekana ni mtu ambaye anakuja na uadilifu wa kuweza kutunza siri. Ni mtu pekee ambaye angeweza kumfuata Slaa na hoja ya kuwa Lowassa anataka kujiunga CHADEMA.

Hapa panaturudisha kwenye swali lile - kwanini Dr. Slaa alikubali kumsikiliza Lowassa akijua ni mtu aliyegubikwa na kashfa za ufisadi? Swali hili siyo sahihi kama wengi wanavyodhania. Swali lililopaswa kuulizwa ni kwanini Gwajima na Lowassa walitaka kuonana na Katibu Mkuu wa CHADEMA ili kumleta Lowassa ndani? Na Katibu Mkuu wa CHADEMA alikuwa na uhuru gani wa kukataa kuonana au kufikisha ombi la Lowassa kwa viongozi wenzake?
Jibu liko wazi – Dr. Slaa alionesha kilele cha busara, uadilifu na uongozi makini. Aliweka hisia zake pembeni, aliweka biases zake pembeni na aliweka hata ujuzi wote alionao kuhusiana na Lowassa pembeni ili kutimiza wajibu wake. Asingeweza kumfukuza Gwajima kuwa amuondolee upuuzi huo, na asingeweza kumkatalia Lowassa bila kuwashirikisha wenzake. Hii ndiyo iliyokuwa hesabu ya Mbowe! Alijua, na alimjua Dr. Slaa kuwa angefanya nini.

Dr. Slaa akitimiza wajibu wake kama Katibu Mkuu wa chama n ahata akiweka pembeni hofu ya kuwa Lowassa angekuja kuchukua nafasi yake ya kugombea alimleta Lowassa mbele ya viongozi wenzake na kutoa nafasi asikilizwe na kama tunavyokumbuka masharti ya upande wake kama Katibu Mkuu. Kitu ambacho hakukijua na wengine wengi hawakujijua ni kuwa Lowassa asingeweza kuja CHADEMA kuwa mpiga debe wa Dr. Slaa, Lowassa asingekuja na kuwa shabiki tu wa CHADEMA. Lowassa alikuwa anakuja kuendeleza – siyo kutafuta – nafasi ya kutimiza ndoto yake kule.

Na hapa ndipo Slaa alipozungukwa na Mbowe na wenzake – ambao waliona tangu zamani kuwa hesabu zao ni bora Lowassa awape nafasi ya kusogelea Ikulu na Uwaziri Mkuu kuliko Slaa. Ndio maana basi – walikuja na maelezo kuwa “utafiti ulionesha Dr. Slaa asingeweza kushinda!”.

Hii ndio siri. Na katika mazingira hayo Dr. Slaa angeweza vipi kuendelea kuwepo pale pale ambapo aliamini hapakupaswa kuwepo? Angeweza vipi kuvuruga matumaini ya Watanzania ya kuwapatia uongozi bora kwa kuchukua kile ambacho alishakionesha kuwa siyo uongozi bora?

Kumbe ukweli ni kuwa MBowe alimzunguka Slaa, akasaliti urafiki na uhusiano wao wa kazi na kwa ajili ya hamu ya yeye pia kutimiza ndoto yake ya Uwaziri Mkuu na wakati huo huo kutimiza ndoto ya Lowassa kuwa Rais. Anajua kuwa hata kama Lowassa hatoshinda, basi CHADEMA safari hii inaweza kabisa kupata wabunge wengi na hivyo kuweza kumpata yeye kama Waziri Mkuu.

Lowassa wakati anajiuzulu alisema tatizo ni Uwaziri Mkuu. Safari hii tunajua pia tatizo ni Uwaziri Mkuu. Ndoto ya Mbowe na ndoto ya Lowassa zimekumbatiana.

Dr. Slaa hakuwa na chance!
Kilele cha usaliti kimekamilika, mabadiliko yameahirishwa kwa miaka mitano!
Aliyeyaahirisha anajulikana.
Weekend njema. Tukutane Jumatatu, InshaaAllah.