Monday, October 12, 2015

Kwa nini Magufuli ataibuka kidedea?

WATANZANIA wanakwenda kupiga kura Oktoba 25 mwaka huu. Huu ni Uchaguzi Mkuu wa kusisimua zaidi na wenye mvuto zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka 1992. 

Miongoni mwa wagombea urais; wawili ndiyo wenye wafuasi wengi zaidi –John Pombe Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema ingawa anaungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa. Tayari taasisi mbili zinazoheshimika hapa nchini zimefanya utafiti unaoonyesha kwamba Magufuli ataibuka kinara kwenye mbio hizo za urais. Kimsingi, tafiti zote mbili (ule wa Twaweza na Synovate) zinampa Magufuli ushindi wa alama zaidi ya 20 kuliko mpinzani wake huyo. Viongozi na wafuasi wa Ukawa wametumia nguvu kubwa kukataa matokeo hayo ya utafiti wa kisayansi kiasi cha wao nao kuibuka na utafiti wa taasisi wanayoifadhili wao wenyewe. Ukawa, wakubali au wakatae, namba huwa hazidanganyi. CCM ilikataa matokeo ya utafiti wa Synovate mwaka 2010 kwa sababu hizo hizo zinazotolewa sasa na wana Ukawa, lakini matokeo yakaja kuwa yanayofanana. Makala hii inataka kueleza kwa nini CCM itaibuka na ushindi kwenye uchaguzi huu na Magufuli ndiye atakuwa Rais wa Tano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 


Kuaminika Tafiti mbalimbali zilizofanyika zimeonyesha kuwa kwa sasa Dk. Magufuli ndiye mwanasiasa anayeaminika zaidi hapa nchini kuliko mwingine yeyote. Utafiti wa IPSOS ulionyesha kwamba katika kila Watanzania kumi, saba wanaamini kwamba Magufuli atatekeleza kile anachoahidi. Wakati huo huo, ni Watanzania watano tu kati ya kumi wanaoamini kuwa Lowassa atatekeleza kile anachoahidi wakati wa kampeni. Hii maana yake ni kwamba, ahadi za Magufuli wakati wa kampeni zinawaingia wapiga kura kuliko ahadi za wagombea wengine. Kwenye siasa, hii peke yake ni faida isiyopingika. Uaminifu huu umejengwa na utendaji kazi wa mwanasiasa huyu katika utumishi wake. Kila alipoahidi kwamba barabara itajengwa, ilijengwa. Alipoahidi kwamba atapambana na wavuvi haramu, alipambana nao. Faida nyingine ya Magufuli kwenye kuaminika kwake ni ukweli kuwa yeye hatokani na historia ya ukada wa chama kama ilivyo kwa Lowassa. Ndiyo maana, kimkakati kabisa, CCM ikaamua kumuuza Magufuli kama alama kuu badala ya chama chake. Magufuli hajakimbia chama chake na wala chama hakijamkimbia. Kilichofanyika ni kujenga mkakati utakaomtofautisha mgombea na chama chake ambacho kwa baadhi ya wananchi ni sehemu ya matatizo ambayo nchi yetu inayo kwa sasa. Kama wananchi wanamwamini Magufuli, kwa mujibu wa tafiti za kisayansi kabisa, maana yake ni kuwa huyo ndiye watakayempigia kura. Magufuli ni mwenzao Zaidi ya nusu ya Watanzania ni masikini. Wananchi hawa wangependa kumwona mmoja wao au mtu wanayeweza kujifananisha naye akipata nafasi ya kuwaongoza. Magufuli anawapa Watanzania matumaini hayo. 

Anatoka katika familia ya kimasikini. Amekulia kwenye umasikini na ndiyo maana kila akienda mikoani haachi kusimulia namna alivyochunga ng’ombe na kuuza maziwa utotoni. Magufuli hahitaji kufanya usanii wa kupanda daladala kuonyesha ukaribu wake na wananchi. Ameuishi umasikini na anajua kero za watu wa kundi hilo. Wananchi hawa masikini watampa Magufuli kura zao kwa sababu wanamwona ni mtu anayejua shida zao. 

Kwa miaka mingi, Lowassa amejitambulisha kama mwanasiasa tajiri aliyezungukwa na genge la matajiri wenziwe. Dunia nzima, katika nchi zinazoendelea, masikini wamekuwa na utaratibu wa kumpigia kura mtu wanayemwona anafanana na hali yao. Kuondoa nchi ambazo watu huchagua katika misingi ya kikabila, kidini na kiitikadi, kwa kawaida mtu anayeonekana wa kawaida hushinda. Hii ndiyo sababu ya Evo Morales kushinda Bolivia, Narendra Modi kupata uongozi India na Jacob Zuma kumshinda Thabo Mbeki ndani ya ANC na hatimaye kwenye urais wa Afrika Kusini. John Pombe Magufuli ni mtumishi wa serikali asiye na mahusiano yanayofahamika na matajiri wenye kashfa, anasomesha watoto wake katika shule wanazosoma wananchi wa kawaida na ana lafudhi ya Kisukuma ambayo kama angekuwa anafanya kazi sokoni Kariakoo, wenzake wangemwita Ngosha na wasingejisumbua kuuliza jina lake halisi. Wapiga kura wanataka mtu wa namna hii wanayeweza kujihusisha naye. Nguvu ya CCM Hakuna shaka kwamba CCM ni miongoni mwa vyama vyenye mtandao mpana zaidi barani Afrika. 

Pamoja na matatizo yaliyopo, lakini CCM kinaweza kujigamba kwamba kina wanachama katika kila wilaya na katika kila kata hapa nchini. Ni wanachama haohao ambao kwa miaka 20 iliyopita wameipa CCM ushindi wa zaidi ya asilimia 60 kila wakati wa Uchaguzi Mkuu. Hakuna chama chochote kingine hapa Tanzania (hata kama ukichukua Ukawa kwa ujumla wao) kinachoweza kujisifu kuwa na mtandao wa namna hii. Ndiyo maana sishangazwi sana na matokeo ambayo yametangazwa na watafiti wa Twaweza na Synovate yanayoonyesha kuwa CCM itashinda kwa zaidi ya asilimia 60. Kuna kundi kubwa la vijana waliojitokeza kujiandikisha mwaka huu lakini idadi yao haiwezi kuzidi wale waliokuwa tayari wamejiandikisha tangu mwaka 2010. 

Ninapoandika makala hii, kwa sababu ya oganaizesheni yake ya ndani, CCM inajua ni wanachama wake wangapi wamejiandikisha na watapiga kura mwaka huu panapo uzima. Huwezi kusema hili kwa wana Ukawa. Nguvu hii ya CCM inafanya kazi ya kujiandaa na kupanga mikakati iwe rahisi na imara. Miongoni mwa vyama vya Kiafrika, haijawahi kutokea kwa chama kilicho na mtandao mpana na chenye nguvu kama CCM kushindwa kwenye uchaguzi. Hali itabaki hivyo mwaka huu. Tabia wapiga kura Wanasayansi ya siasa wanaamini kwenye tabia fulanifulani za wapiga kura. Ndiyo maana, nchini Marekani, kuna majimbo yanajulikana kuwa ni ya bluu na mengine mekundu. Kwamba hayo majimbo miaka yote hupigia kura Republican au Democrat. Nchini Tanzania, tafiti zilizofanyika huko nyuma zimeonyesha kuwa wapiga kura wa CCM wana tabia moja inayofanana kwamba huwa wanampigia kura mgombea wao. Kama walikuwa wanakupenda ulipokuwa CCM, ukihama watampa yule wa chama chao. 

Hii maana yake ni kuwa mgombea wa Ukawa, Lowassa, ambaye alikuwa CCM, hatapata kura nyingi kutoka CCM kama anavyodhani. Bahati nzuri ni kwamba Magufuli ni mgombea anayekubalika na wana CCM wengi. Kimsingi, waziri huyu wa ujenzi alikuwa anapendwa zaidi nje ya chama kuliko ilivyokuwa ndani ya chama chake. Kwa mwana CCM wa kawaida ambaye hakukosa chochote baada ya Lowassa kunyimwa urais (achana na akina Kingunge, Guninita na Mgeja), Magufuli ni aina ya mgombea waliyekuwa wanamtaka. Kura za wana CCM zitakwenda kwa mgombea wao. Lowassa anaweza kupata kura za hapa na pale za wana CCM lakini nadhani Magufuli pia atapata kura za wana Ukawa ambao hawamwoni huyu bwana kama mtu anayeweza kuleta mabadiliko. 

Kama ilivyokuwa kwa Dk. Wilbrod Slaa na Profesa Ibrahim Lipumba, wapo wananchi wanaoamini kuwa Ukawa ilikosea kumpitisha Lowassa. Hawa, itakapofika siku ya kupiga kura, watampa Magufuli kura zao. Lowassa anaumwa Habari ambayo haisemwi sana siku hizi ni kwamba wananchi wengi zaidi sasa wamemwona Lowassa na kubaini namna anavyoonekana kuwa na matatizo ya kiafya. Wanamwona mgombea anayezungumza kwa dakika tatu na kutembea kwa shida. Ni jambo lingine kusikia tetesi lakini kumwona mtu kwa macho yako ni jambo lingine kabisa. Taarifa kutoka mikoani na maeneo kama Geita, zimeonyesha kuwa wengi wa wananchi wamefadhaishwa na hali ya kiafya waliomwona nayo Lowassa. Mijini ni rahisi kuwaambia watu kuwa Ikulu hakuhitaji misuli. Lakini, kwa wananchi wa vijijini ambako Lowassa amekwenda kuomba kura, afya njema ni kila kitu. Hawa wananchi wanaishi kwa kazi za suluba na namna pekee ya kupeleka mkono kinywani ni kuwa na afya njema. 

Wamemwona Lowassa na habari kutoka mashambani ni kwamba wengi wamebaini kuwa mgombea wa Ukawa ana matatizo ya kiafya. Hali hiyo ni tofauti na Magufuli ambaye anazungumza kwa wastani wa saa moja kwenye mikutano yake. Anatembea kwa gari kwenye barabara zenye vumbi na wananchi wanamwona alivyo fiti kwa zile pushapu zake na ule wimbo wake wa vita wa ARISELEMA ! Vijijini kuna wananchi wengi kuliko mijini. Na hawa wameona tayari nani ana afya ya kuwaletea mabadiliko wanayoyataka. Ni Mgufuli na ndiyo maana ataibuka mshindi Oktoba. Bao la mkono Wasomaji wa magazeti watakuwa wamebaini kuwa vyombo hivyo vya habari vinasaidia zaidi Ukawa kuliko CCM. Mengi ya magazeti makubwa hapa nchini yanamilikiwa na viongozi au wafadhili wa Ukawa. Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, anamiliki gazeti la Tanzania Daima ambalo safari hii limejipambanua waziwazi kama gazeti la Ukawa. Reginald Mengi na Rostam Aziz wanamiliki magazeti ya Nipashe na Mtanzania na uhusiano wao wa karibuni unajulikana. CCM imebaki na Uhuru lake. Hata hivyo, chama tawala kimefanikiwa kupiga kile ambacho Katibu Mwenezi wake, Nape Nnauye, angekiita ‘bao la mkono’. Kwa kufahamu kuwa itazidiwa magazetini, CCM imeamua kutumia zaidi televisheni na redio kwenye kampeni zake za mwaka huu. 

Mikutano yote mikubwa aliyofanya Magufuli mikoani imeonyeshwa kwenye televisheni. Matokeo yake, mtu ambaye alikuwa haonekani maarufu kulinganisha na Lowassa, sasa anajulikana hadi na watoto. Kama angetegemea magazeti kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, Magufuli angekuwa ameachwa mbali. Kwa bahati nzuri, CCM pia inaonekana kuwekeza kwenye eneo la mitandao ya kijamii ambako kwenye miaka ya nyuma haikuweka mkazo sana. Matokeo yake, CCM na Magufuli sasa wamejitangaza vizuri kwa vijana. 

Televisheni, redio na mitandao inawafikia watu wengi zaidi kuliko magazeti. Kwa siku, Tanzania inachapa nakala zisizozidi 200,000 za magazeti na wasomaji wasiozidi milioni moja kwa ujumla. Kupitia televisheni, redio na mtandao, mwanasiasa anaweza kupeleka ujumbe hadi kwa watu milioni 10 kwa siku. Hili ndilo bao la mkono alilolisema Nape Nnauye ! 

Inaonekana Ukawa hawajaijua siri hii hadi sasa ! Mwandishi wa makala haya Sigfrid Urassa, aliyejitambulisha kama msomaji wa Raia Mwema 

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/kwa-nini-magufuli-ataibuka-kidedea#sthash.D8TuDHAJ.dYbYUfry.dpuf
Gazeti la Raia Mwema

No comments:

Post a Comment